Saturday, May 18, 2013

Wizara ya Maji inahitaji Sh.bilion 4.6 kusomesha wataalamu wa maji.


Ruth Mnkeni na Aziza Juma, Dar es Salaam.

JUMLA ya Sh.bilioni 4.6 zinahitajika  kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi wa walio vyuoni ili kuboresha maendeleo katika sekta ya maji nchini.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe wakati wa kuzindua Mfuko wa Udhamini wa Maji (WTF)  ambao unawasomesha wanafunzi wanaochukua taaluma ya sekta ya maji.

Profesa Maghembe alisema kuwa mfuko huo utasaidia kuboresha sekta hiyo kwani mahitaji ya maji ni makubwa katika maisha ya binadamu.

Aliongeza kusema kuwa wanao mpango mkakati wa kusambaza maji katika maeneo ya vijijini kwani kuna vyanzo vingi ijapokuwa vinaathiriwa na watu wachache kwa manufaa yao binafsi .

“Kuna watu ambao ni wezi wa maji wanajitengenezea visima wakidai kuwa vinatoa maji kumbe wanatumia maji ya DAWASCO lakini tulifanya operesheni ya miezi mwili na tuliwakamata zaidi ya watu 90 ambao walikuwa wanaiba maji,”alisema

“Juhudi hizi zimepelekea sehemu nyingi katika jiji la Dar es Salaam kupata maji tofauti na ilivyokuwa awali kwani baadhi yao wamehukumiwa na wengine kesi zinaendelea katika mahakama ya jiji .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mfuko huo Dayana Mwiru alisema lengo la kuanzisha mfuko huo ni kujaribu kuongeza idadi ya wanataaluma wa sekta ya maji kwani ni wachache mno.

Alisema utafiti uliofanywa mwaka 2011 ulionyesha kuwa mahitaji ya maji yanahitaji wanataaluma 3000 ili kuweza kufanya kazi ipasavyo tofauti na sasa ambapo haikidhi kwani kuna chuo kimoja tu kinachotoa taaluma hiyo na kwa sasa kuna wanafunzi 1600 ambao wapo kwenye taaluma hiyo.

“Mfuko huu utasaidia kwenya idadi ya wanafunzi kwa kuangalia usawa wa jinsia, watu wanaotoka katika familia duni na pia  wanawake kuwapa kipaumbele ili kuhakikisha kuwa wanafikia malengo bila kujali anatoka katika falimilia gani,”alisema Mwiru.

No comments:

Post a Comment