Thursday, June 6, 2013

Rasimu ya Katiba : Mawaziri wapewa ruksa kukaimu urais

Dar es Salaam. Kutokana na rasimu ya Katiba Mpya kupendekeza kufutwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu, rasimu hiyo inapendekeza waziri yeyote mwandamizi ateuliwe kukaimu nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa rais na makamu wake hawapo nchini kutokana na sababu zozote zile.
Mapendekezo hayo ni tofauti na Katiba ya sasa ambayo inatamka kwamba ikiwa Rais na Makamu wake hawapo, basi nafasi hiyo ya juu katika nchi itashikwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu aliwekwa katika orodha ya wanaoweza kukaimu nafasi hiyo katika marekebisho ya Katiba yaliyofanywa mwaka 2000 kupitia waraka maalumu wa Serikali (white paper) na baadaye kupitishwa na Bunge.
Kabla ya marekebisho hayo ya 13, Ibara ya 37(3)(a) na (b) ilikuwa ikieleza kuwa iwapo Rais na Makamu wake hawapo nafasi hiyo ilitakiwa kushikiliwa na Spika wa Bunge na kama hayupo basi Jaji Mkuu wa Tanzania ndiye alitakiwa kukaimu nafasi hiyo.
Lakini mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya katika Ibara ya 73(1)(b)na (c) inaeleza kuwa endapo Rais na Makamu wake hawatakuwapo basi nafasi hiyo itashikiliwa na waziri mwandamizi na kama hatakuwapo basi Baraza la Mawaziri ndilo litakalokuwa na dhamana ya kuchagua mtu wa kukaimu nafasi hiyo.
Hata hivyo, mtu yeyote atakayekaimu nafasi ya madaraka ya Rais, kwa namna yoyote ile, hatakuwa na madaraka ya kuteua au kumwondoa madarakani kiongozi yeyote yule aliyeteuliwa na Rais kwa mujibu wa Katiba au jambo jingine lolote kama litakavyoainishwa na Rais katika hati ya kukasimu madaraka yake.

“Rais atakasimu madaraka yake kwa hati maalumu aliyotia saini yake,” inaelekeza rasimu hiyo iliyozinduliwa Jumatatu wiki hii na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Kadhalika rasimu hiyo inaeleza kuwa endapo Baraza la Mawaziri litaona kuwa Rais hawezi kumudu kazi zake kwa sababu ya maradhi ya mwili au akili, linaweza kuandaa azimio la kumwomba Jaji Mkuu athibitishe kwamba Rais, kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili, hawezi kumudu kazi zake.
“Baada ya kupokea azimio hilo, atateua bodi ya utabibu ambayo itachunguza suala hilo na kumshauri Jaji Mkuu ipasavyo,” inaelekeza rasimu hiyo.
Jaji Mkuu baada ya kutafakari ushauri na ushahidi wa kitabibu, atampelekea Spika hati ya kuthibitisha kwamba kutokana na maradhi ya mwili au akili, Rais ameshindwa kumudu kazi zake, na iwapo Jaji Mkuu hatabatilisha hati hiyo ndani ya siku saba kutokana na Rais kupata nafuu na kurejea kazini, basi itahesabiwa kwamba kiti cha Rais kipo wazi.
Kutokana na hali hiyo, bodi ya utabibu itakayoteuliwa kwa mujibu wa Katiba itajumuisha watu wasiopungua watatu kutoka miongoni mwa madaktari bingwa wanaotambuliwa na sheria inayohusu madaktari ya Tanzania.
“Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi, kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au akili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na kushika madaraka ya Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano,” inaeleza sehemu nyingine ya rasimu hiyo.

TRA yawapa elimu Wawekezaji wa China.



Aziza Juma na Vick Kanje ,Dar es Saalam

AFISA mwandamizi wa  Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA )Hamisi Lupenja amewataka wawekezaji kutoka Nchi ya China   kupewa elimu ya uwekezaji wa majengo na ujenzi.

Akizungumza katika semina hiyo jana  jijini Dar es Saalm, Lupenja  alisema kuwa lengo la kutoa semina hiyo ni kutoa elimu kwa wawekezaji wa majengo na ujenzi na pia kuboresha mfumo wa kodi.

‘Tupo na jamii ya Wachina tunawapa elimu kuhusu kodi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya upangishaji na kufuata sheria za nchi.

‘Jukumu letu la msingi ni kuwapa elimu ili kuwawezesha kufanya biashara zao kwa ufanisi zaidi ’alisema Lupenja.

Lupenja alisema kuwa wameshafanya semina nyingi na sehemu mbalimbali ikiwemo semina kutumia machine ya Electronic kwa wafanyabiashara .

Alisema kuwa wapotayari kukumbana na changamoto wakati wa utoaji elimu kwa wafanyabiashara na kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaojua kutumia mashine hizo lakini wanakuwa wabishi kutumia wakidai hawajui jinsi ya kutumia .

MWISHO.

Hata hivyo alisema kuwa wanatoa elimu kwa wafanyabiashara wote bila kujali ni Mchina au Mtanzania. 

Mkuu Wa Mkoa Dar ataka wananchi waishio mabondeni wasipimiwe viwanja vyao.



Adelina Rutale na Maneno Selanyika,Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick amewataka viongozi wa mipango miji kutokuwapimia viwanja wananchi maeneo ya mabondeni ambayo ni hatari kwa maisha yao baada ya mafuriko kutokea.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kuhitimisha siku ya maadhimisho ya Mazingira Duniani Sadick alisema kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakijichukulia sheria ya kupima viwanja maeneo ya mabondeni kinyume na sheria.

Pia alisema kuwa wananchi wamekuwa mstari wa mbele kuharibu mazingira kwa kuchimba michanga na kokoto maeneo mbalimbali ya hapa Dar es salaam na kusababisha adha ya mazingira kuwa machafu.

“Viongozi wa mipango miji wajitahidi kusimamia kazi yao,waache kuwapimia wananchi maeneo ya mabondeni huko mafuriko yakitokea yanasababisha hasara kubwa ya mali kupotea na binadamu kupoteza maisha yao,

“Watu wengi wanalalamika Dar es Salaam kuchafu lakini waharibifu ni wao wenyewe hakuna mtu mwingine,tukiamua kuyatunza mazingira tunaweza kuwa na sifa kama mikoa mingine ambayo ibnasifika kwa usafi,”alisema Sadick.

Hatahivyo Sadick alisema kuwa viongozi wasimamie sheria za kutunza kwa kutimiza wajibu wao wa uwajibikaji,taasisi kuitekeleza sheria namba 20 ya mwaka 2004 kama inavyoagiza ya kutunza mazingira.

“Watendaji kupanga matumizi ya ardhi kwa uadilifu kulingana na sifa za ardhi husika mfano kutoruhusu ujenzi mabondeni,ufukweni na utengaji wa maeneo kwa shughuli mbalimbali za kijamii,

“Wananchi kutokupenda kutii sheria zilizopo kwa hiari bila shuruti,usimamizi hafifu na usioridhisha wa sheria ndogondogo na hifadhi ya mazingira,”alisema Sadick.


Pia alisema kuwa kila mwananchi wa mkoa huu watafakari kwa kina juu ya shughuli za uzalishaji wa kiuchumi zunazozingatia utunzaji wa mazingira kwani ni muhimu kuwa na mazingira endelevu kama nchi nyingine.

Aidha viongozi mbalimbali walihudhulia kwenye siku hiyo ikiwemo mkuu wa wilaya,wakurugenzi,madiwani,wenyeviti na wadau mbalimbali kutoka asasi zisizo za kiserikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtandao wa uthibiti wa mabadiliko ya tabia ya nchi (FOFUM CC), Euster Kibona, alisema wamejitahidi kufanyakazi na jamii nzima hasa katika maeneo ya mijini na vijijini kufanya shughuli za uzalishaji kwa maendeleo endelevu bila kuathiri mazingira.

Alisema kuwa maeneo ya miji ambako kuna viwanda vingi ndiko kunakoonekana kuathirika zaidi na uchafuzi wa mazingira kutokana na hewa inayotoka viwandani, maji machafu na taka nyingine nyingi.

“Kulinda na kutunza mazingira ni jukumu la mimi wewe na sisi hivyo tunatakiwa kila mmoja kuchukua hatua kuanzia sasa ili kuondokana na maginjwa yasiyotarajiwa kama vile ya mlipuko na mengine,” alisema Kibona.

Wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi waishauri TRA kupunguza bei ya mashine za kutolea risiti.



Na Aziza Juma, Dar ea Salaam.

WAFANYABIASHARA wa vifaa vya ujenzi wameishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupunguza bei ya mashine za kutolea risiti ili wafanyabiashara wote kumudu kununua mashine hizo.

Akizungimza na MTANZANIA jana  mmoja wa wafanyabiashara hao Matchowea Malisa katika semina ya wafanyabiashara inayoendelea katika wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Malisa alisema kuwa wafanyabiashara wengi wanatumia mikopo kuendesha biashara zao hivyo itakuwa vigumu kutafuta rejesho la mkopo benk wakati huhuo anatakiwa kununua mashine ambayo inauzwa bei  kubwa kiasi cha laki nane.

Alisema pamoja mashine zina faida kubwa na nyingi sana lakini zinafanya kazi taratibu sana hali inayopelekea ugumu wateja wanapokiwa zaidi ya wawili.

Pia Malisa alisema kuwa watengenezaji wa bedhaa na wafanyabiashara wa jumla waseuza rejareja bidhaa wanazotengeneza ili kuwapa nafasi ya wale wanaouza rejareja tu waweze kuuza kwani wateja wote wanakimbilia huko kwakua bei yao ya chini sana.

Aliongezea kuwa msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara wenyemtaji mdogo usiozidi milioni nne unapunguza uzalendo kwani watakuwa hawana uchungu na nchi yao pia hawato changia
ongezeko la pato la Taifa.

TRA kuwazungukia wafanyabiashara Dar kutoa elimu.


Na Aziza Juma, Dar es Salaam.

MAMLAKA  ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kuanza mkakati wa kuwazungukia wafanyabiashara katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam lengo likiwa ni kutoa elimu juu ya matumizi ya mashine ya kutolea risiti.

Akizungumza na MTANZANIA jana Afisa mwandamizi wa elimu wa TRA Hamisi Lupenja ziara hiyo itaanza baada ya kumaliza semina inayoendelea  kwa wafanyabiashara hao.

Lupenja alisema mafunzo haya yanawalenga wale wafanyabiashara wenye pato la zaidi ya milioni 14 kwa mwaka na hasa wafanyabiashara ya vifaa vya ujenzi, nguo, vipuri, baa na hoteli.

“Mafunzo hayo ni kwajili ya faida kwa wafanyabiashara sio kwa TRA tu kwani inasaidia kutunza  kumbukumbu za mauzo na kudhibiti ubabaishaji wa wasaidizi wao hata wakisafiri” alisema Lupenja.

Kwaupande wake mfanyabiashara wa vipuri  Hanifa Adam aliipongeza TRA kwa hatua waliyoifanya kwani imewajengea uwelewa wa kutosha juu ya matumizi ya mashine hizo.

“Tunaishukuru TRA kwa mafunzo haya kwani yametusaidia sana katika kutumia na kujua umuhimu wa mshine hizi” alisema Hanifa.